Mapinduzi Cup: URA waiondoa Simba mashindanoni

Timu ya Soka ya Simba SC imeyaaga rasmi mashindano ya Mapinduzi Cup baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 kutoka watoza ushuru wa Uganda URA.

Simba walikuwa wakihitaji ushindi wa aina yoyote ile kufuzu  Hatua ya nusu fainali lakini hali ilikuwa tofauti katika mchezo huo ambao umefanyika katika uwanja wa Amaan Visiwani Zanzibar.

Bao pekee la URA katika mchezo huo limefungwa na Deboss Kalama katika dakika ya 43 ya kipindi cha kwanza bao ambalo lilidumu hadi kipyenga cha mwamuzi Mfaume Ally Nassoro kilipopulizwa kuashiria dakika 90 kumalizika.

URA wanaungana na Azam kutoka kundi A pamoja na Singida United na Yanga ambao wanafuzu kupitia kundi B.

Vinara kundi A. 

Baada ya ushindi huo URA wanakwenda kileleni mwa Kundi A wakiwa na alama 10 wakifuatiwa na Azam FC ambao wana alama 9.

URA watasubiri kujua mpinzani wao katika nusu fainali baada ya mchezo wa kumaliza kundi B kati ya Singida United na Yanga utakaopigwa kuanzia saa mbili na nusu usiku huu.